Askari
Polisi wakiwa wananyofoa mimea ya bhangi ambayo ilikuwa imepandwa
kwenye moja ya shamba lililopo katika kijiji cha Kismiri Juu kata ya
Uwiro tarafa ya King'ori wilayani Arumeru.
(Picha na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha)
Askari
wa Jeshi la Polisi wakiteketeza magunia ya bhangi kwa kuchoma moto mara
baada ya kuyakusanya kutoka kwenye moja ya nyumba ya mkulima wa zao
hilo haramu eneo la kismiri Juu wilayani Arumeru.
(Picha na Rashid
Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha).
Askari
wa Jeshi la Polisi wakitoa magunia ya bhangi katika moja ya nyumba
iliyopo katika kijiji cha Engalaon kata ya Mwandeti tarafa ya Muklati
wilayani Arumeru mara baada ya wenyeji kukimbia na kuacha mlango. (Picha
na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
.........................................................................................
Na
Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Pamoja na Jeshi la
Polisi mkoani hapa kufanikiwa kuongeza takwimu za ukamataji wa madawa ya
kulevya kwa makosa 75 zaidi kwa mwaka 2016 kulinganisha na mwaka 2015,imeonekana
kwamba mwaka huu 2017 kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Usalama pamoja na Tume
ya Kuratibu na Kudhibiti dawa za kulevya nchini, kasi hiyo ya kuthibiti kilimo
cha madawa ya kulevya aina ya bhangi ambacho kinalimwa baadhi ya maeneo ya
wilaya ya Arumeru imeanza mapema.
Akizungumza na waandishi
wa habari ofisi kwake mara baada ya operesheni ya kutokomeza madawa hayo kufanyika
kwa siku mbili, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles
Mkumbo alisema kwamba Jeshi hilo pamoja
na vyombo vingine limeamua kuanza kuharibu mimea iliyopo mashambani mapema hasa
kipindi hiki cha masika ambapo uoteshaji ufanyika ili kazi ya kudhibiti madawa
hayo huko mbeleni iwe rahisi.
Kamanda Mkumbo
alisema katika operesheni hiyo jumla ya hekari 31 za mimea ya bhangi
ziliharibiwa huku gunia 58 na kilogramu 210 ziliteketezwa kwa moto katika
maeneo ya kijiji cha Kismiri Juu kata ya Uwiro tarafa ya King’ori na katika
kijiji cha Engalaon kata ya Mwandeti tarafa ya Muklati wilayani Arumeru.
“Siku ya kwanza
Jumanne tarehe 10.01.2017 Operesheni hiyo ilifanyika katika kijiji cha Kismiri
Juu kata ya Uwiro tarafa ya King’ori na kupata jumla ya magunia 31 ya bhangi na
kilogramu 210 za mbegu zilipatikana huku hekari 19 za mimea hiyo ziliharibiwa”.
“Siku ya tarehe
12.01.2017 Alhamisi operesheni hiyo iliendelea tena katika maeneo ya kijiji cha
Engalaon kata ya Mwandeti tarafa ya Muklati na kufanikiwa kupatikana kwa
magunia 27 na kuharibu hekari 12 za mimea ya bhangi hivyo kufanya jumla ya magunia
58 kupatikana, mbegu kilogramu 210 kupatikana na hekari 31 za mimea huo
kuharibiwa”. Alifafanua Kamanda Mkumbo.
Kamanda Mkumbo
alitoa onyo kali kwa viongozi wanaoishi au kufanyia kazi maeneo hayo, kuacha
mara moja kuwaunga mkono wakulima wa bhangi.
"Jeshi la Polisi mkoani hapa linawaonya
viongozi wa maeneo ambayo zao hilo linalimwa kuacha mara moja kuwaunga mkono
wakulima hao, naamini ulimaji mpaka uuzaji wa bhangi unafanywa kwa uwazi katika
maeneo hayo bila wao kuchukua hatua”.
“Watambue kwamba wao
ni walinzi wa amani katika maeneo yao na washirikiane na Jeshi la Polisi katika
kutokomeza kabisa kilimo hicho cha bhangi ambayo inaleta madhara makubwa kwa
jamii hasa kundi la vijana”. Alisisitiza Kamanda Mkumbo.
Naye mkuu wa kitengo
wa kuthibiti dawa za kulevya nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la
Polisi(SACP) Mihayo Msikhela alisema Jeshi la Polisi nchini limejipanga hasa
kwenye kuzuia kuliko kutibu ndio maana wameamua kuharibu mapema mimea ya zao
hilo haramu kabla ya kukomaa na kusambaa.
Alisema kwamba kiwango
cha uteketezaji wa dawa za kulevya hapa nchini kwa mwaka 2016 kiliongezeka ikilinganishwa
na mwaka juzi 2015.
Kwa upande wake
Afisa sheria mkuu toka Tume ya Kuratibu na Kuthibiti dawa za kulevya Bi.
Christina Gervas alisema kwamba kadri bajeti itakaporuhusu watazidi
kushirikiana na vyombo vya Usalama kufanya operesheni mara kwa mara katika
maeneo ambayo bhangi inalimwa na pia kuahidi kutoa elimu kwa wakulima na
viongozi wa maeneo hayo ili waweze kuachana na zao hilo haramu na kujikita
kwenye mazao halali ya chakula na biashara.
No comments:
Post a Comment