Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amekabidhi
shilingi milioni 5 ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake aliyoitoa alipotembelea ujenzi
wa kituo hicho cha polisi tarehe 13.11.2017 na wananchi kumuomba kuchangia
ambapo ukamilifu wa kituo hicho utasaidia kuhudumia kata 13 zilizopo katika
bonde la ziwa Rukwa.
Sambamba na hilo Mh. Wangabo pia aliwasilisha ahadi ya
Milioni 10 aliyoitoa Mkuu wa jeshi la Polosi nchini IGP Simmon Siro alipotemblea
Mkoa wa Rukwa na kuongeza kuwa kuna shilingi milioni 1.5 ambayo pia ni ahadi ya
mkazi wa bonde la ziwa Rukwa anayeishi nje ya Mkoa ambaye hakuhitaji kutajwa
jina lake.
“Nimekuja kutekeleza ahadi yangu ambayo inaendana na
mlichonisomea, mlisema ili kituo cha polisi kikamilike mlihitaji shilingi
milioni 4, mkaniomba niwatafutie, mimi nimekuja na shilingi milioni 5, ila
nilituma timu yangu ili kuangalia ile gharama kama ilikuwa sahihi, nikaambiwa
na hiyo timu kuwa inahitajika shilingi Milioni 22, alipokuja Kamanda IGP
niliteta nae na alipoona umuhimu wa kituo hiki aliahidi shilingi Milioni 10,”
Mh. Wangabo alisema.
Wakati akikabidhi fedha hizo kwenye mkutano na wananchi niaba
ya Mkuu wa Mkoa, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa Albinus Mgonya alimtaka Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Hamis Mongela kukiri kupokea
fedha hizo huku ahadi nyingine zikiendelea kufuatiliwa ili ujenzi wa kituo
hicho ukamilike kwa wakati, nae Hamisi alikiri kupokea fedha hizo.
Diwani wa kata ya Mtowisa Mh. Edgar Malinyi alisema kuwa ujenzi
wa kituo hicho ni juhudi za wananchi wanaotaka usalama wa vitu na mali zao
wakishirikiana na polisi huku mtendaji wa Kata ya Mtowisa Paulo Katepa akisesama
kuwa wananchi hawatakata tamaa hadi kituo hicho kikamilike kwani ujezi wake
ulianza tangu mwaka 2002.
IMETOLEWA NA
OFISI YA MKUU WA MKOA WA RUKWA

0 Comments