Mhe. Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson akimsikiliza Daktari Bingwa wa upasuaji wa Moyo kwa Watoto na Mkuu wa Idara ya Upasuaji wa Moyo kwa Watoto Godwin Sharau alipotembelea leo chumba cha upasuaji wa Moyo kilichopo Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwetwe (JKCI).
Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Ackson ameahidi kununua luninga mbili ambazo atazikabidhi kwa uongozi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Dk. Tulia ametoa ahadi hiyo leo alipofanya ziara ya kuwafariji wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo hasa watoto ambao wanasubiri kufanyiwa upasuaji.
Amepata fursa pia ya kumjulia hali mtoto Doreen Sostenes (3) ambaye gharama zake za matibabu yake zimelipiwa na Tulia Trust Fund ambayo anaisimamia.
“Nimefika hapa na kujionea changamoto kadhaa ambazo zinawakabili JKCI, nimewatembea watoto wodini”.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Dk. Tulia amesema luninga hizo zitafungwa katika wodi mbili za watoto hospitalini hapo.
“Nimekwenda wodini kuwajulia hali watoto, wamelazwa wakisubiri kufanyiwa upasuaji, binafsi nimeguswa kununua luninga mbili ambazo naamini zitasaidia kuwafariji wakiwa wamelazwa wodini wakisubiri matibabu yao,” amesema.
Ametoa wito kwa viongozi wengine kutembelea Taasisi hiyo na kusaidia kulipia gharama za matibabu ya watoto wanaosumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kusaidia kutatua changamoto nyingine zilizopo hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment